WANUFAIKA WA UPANDIKIZWAJI FIGO, ULOTO WAISHUKURU SERIKALI YA TANZANIA

Published: May 08, 2026
WANUFAIKA WA UPANDIKIZWAJI FIGO, ULOTO WAISHUKURU SERIKALI YA TANZANIA cover image
Na. Jeremiah Mbwambo na Jeremia Mwakyoma
Picha:Gladys Lukindo
 
DODOMA - MEI 6, 2026
 
 
BAADHI ya wananchi walionufaika na huduma za upandikizaji figo na uloto katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamin Mkapa (BMH), wameishukuru serikali pamoja na madaktari kwa kuwawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya matibabu hayo.
 
 
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kwanza wa kimataifa wa huduma za upandikizaji viungo hapa nchini ulioandaliwa na BMH ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); mmoja wa wanufaika wa upandikizaji figo, Richard Masimba, aliyepandikizwa figo miezi sita iliyopita, alisema huduma hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika afya yake na kumpa matumaini mapya ya maisha.
 
 
Masimba aliishukuru BMH na serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya upatikanaji wa matibabu hayo nchini, akisisitiza kuwa hatua hiyo imeokoa maisha ya wengi waliokuwa wakisumbuliwa na maradhi ya figo.
 
 
Aidha, aliitaka jamii kutokata tamaa wanapokumbwa na changamoto za kiafya, hususan magonjwa ya figo, akieleza kuwa matibabu yapo na yanaweza kusaidia kurejesha afya iwapo yatatafutwa kwa wakati.
 
 
Kwa upande wake, Naira Gwota aliyenufaika na upandikizaji uloto na kupona ugonjwa wa Sickle Cell aliwashukuru madaktari kwa juhudi zao za kumhudumia hadi kufanikisha matibabu hayo.
 
 
Alisema kabla ya kufanyiwa upandikizaji huo, alikuwa akiugua mara kwa mara hali iliyomlazimu kukosa masomo kutokana na kulazwa hospitali kila wakati.
 
 
Hata hivyo, alieleza kuwa baada ya kufanyiwa upandikizaji uloto, hali yake imeimarika kwa kiasi kikubwa na sasa anaendelea vizuri na masomo yake, jambo lililorejesha matumaini yake ya kufikia ndoto zake za maisha.