TUJITOKEZE KUPIGA KURA OKTOBA 29
Na Ludovick Kazoka,Dodoma: OKTOBA 27
Wananchi wameombwa kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi katika uchaguzi mkuu unaofanyika tarehe 29 Oktoba.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
"Hii ni sehemu ya maadhimisho yetu (Hospitali ya Benjamin Mkapa) ya miaka 10. Matembezi haya ni kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, baada ya kumaliza matembezi ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kutekeleza haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
Matembezi hayo yalijumuisha watumishi wa BMH na UDOM.
Kwa mujibu wa Prof Makubi, matembezi hayo yanaonyesha umoja uliopo baina ya Hospitali ya Benjamin Mkapa na Chuo Kikuu cha Dodoma.
"UDOM ndiyo waasisi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa. Hivyo matembezi haya ya pamoja ni kwa ajili ya kuendeleza umoja wetu," ameongeza.
Kwa upande wake, kaimu Makamu Mkuu wa UDOM, Prof Albino Tenge, amesema matembezi hayo ya pamoja ni kwa ajili ya kuwapongeza BMH kwa kutimiza miaka 10 ya huduma.
"Matembezi haya pia ni kwa ajili ya kuhamasisha wananchi wajitokeze kwenda kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu siku ya Jumatano hii," amesema Prof Tenge.