TUANZISHE HUDUMA MPYA AMBAZO NI ZA UPEKEE (UNIQUE) : PROF ABEL MAKUBI
Na Ludovick Kazoka
Idara mbalimbali za huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wametakiwa kuja na huduma mpya ambazo hazipo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, akizitaka idara za huduma zianzishe huduma ambazo ni unique (za pekee).
"Huduma hizi zitavutia wateja ndani ya nchi na kutoka nje ya nchi hivyo kuongeza idadi ya wateja," amesema Mkurugenzi Mtendaji wakati akifungua kikao cha Watumishi wote wa BMH leo Alhamisi.
Prof Makubi ametumia mkutano huo kuwapongeza watumishi wa BMH kwa ongezeko la wateja kutoka 1000 mpaka 1300 kwa siku.
"Sasa hivi tunahudumia wananchi 1300 kwa siku kutoka 1000 tuliokuwa tunahudumia zamani. Hili ongezeko ni kutokana na jitihada zenu. Tunapata wateja kutoka Kanda ya Kati pamoja mikoa ya jirani," ameongeza.
Prof Makubi aliongeza kuwa miradi ambayo ipo mbioni kuanzishwa ni Kituo cha Matibabu cha Figo ambacho kitagharimu B28 na kwamba kitajengwa na wadau wa BMH kutoka Japan.
"Tunawashukuru wadau wetu Shirika la Tokushukai kutoka Japan kwa kugharamia mradi huu na pia walitusaidia kuanzisha huduma ya upandikizaji figo," amesema Prof Makubi.