SERIKALI YA MALAWI YAPONGEZA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUTOA HUDUMA ZA UPASUAJI BURE KWA WAGONJWA 294

Published: Oct 26, 2026
SERIKALI YA MALAWI YAPONGEZA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWA KUTOA HUDUMA ZA UPASUAJI BURE KWA WAGONJWA 294 cover image
Serikali ya Malawi imeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa huduma za upasuaji wa kibingwa bila malipo kwa wagonjwa 294 wakati wa kambi ya matibabu iliyodumu kwa wiki mbili katika Hospitali ya Rufaa ya Mzuzu na Hospitali ya Rufaa ya Kamuzu.
 
 
 
Kambi hiyo ilifanyika kuanzia Septemba 28 hadi Oktoba 9, 2026, ikihusisha madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya Tanzania. Lengo la kambi hiyo lilikuwa kuimarisha ushirikiano wa sekta ya afya kati ya nchi hizo mbili, kuwezesha kubadilishana ujuzi na kuongeza uwezo wa wataalamu wa afya wa Malawi katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa.
 
 
Akizungumza katika hafla ya kufunga kambi hiyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kamuzu siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Utawala katika Wizara ya Afya na Usafi wa Mazingira ya Malawi, Bestone Chisamile, alisema kuwa mpango huo umewezesha utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwa kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wagonjwa na wataalamu wa afya.
 
 
Alipongeza timu ya madaktari kutoka Tanzania kwa kushirikishana utaalamu, kuhamisha ujuzi na kuimarisha uwezo wa wataalamu wa afya wa Malawi kupitia utoaji wa huduma za kibingwa na ushirikiano wa kitaaluma.
 
 
Timu hiyo ilitoa huduma za upasuaji wa ubongo na uti wa mgongo, mifupa, upasuaji wa jumla, magonjwa ya moyo na mfumo wa mkojo, pamoja na tathmini kwa wagonjwa wanaohitaji kupandikizwa figo na uboho. Huduma zote zilitolewa bila malipo. Hospitali ya Rufaa ya Mzuzu pekee ilirekodi jumla ya upasuaji 108.
 
 
Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Richard Kayola, alisema kuwa kambi hiyo ilitekelezwa kwa mujibu wa Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano iliyosainiwa na nchi hizo mbili mwezi Machi 2025.
 
 
Aliwahimiza wananchi wa Malawi wanaohitaji huduma za matibabu ya kibingwa kufahamu na kutumia fursa ya huduma zinazotolewa na Hospitali ya Benjamin Mkapa nchini Tanzania.
 
 
Alibainisha kuwa makubaliano hayo ya nchi mbili yanatoa fursa ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kibingwa na kupunguza gharama zinazohusiana na kutafuta huduma kama hizo katika nchi nyingine za nje.
 
 
Mpango huo unadhihirisha dhamira ya Serikali za Malawi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuimarisha ushirikiano wa afya baina ya nchi hizo mbili, kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani na kuboresha upatikanaji wa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.