WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI WATEMBELEA BMH, WAPONGEZA UWEKEZAJI  SEKTA YA AFYA

Published: Jul 04, 2026
WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI WATEMBELEA BMH, WAPONGEZA UWEKEZAJI  SEKTA YA AFYA cover image

Na Gladys Lukindo
DODOMA - JUNI 25, 2026

Wahariri wa vyombo vya habari leo wamefanya ziara katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) na kupongeza uwekekezeji mkubwa uliofanywa kwenye sekta ya Afya hususani katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.


Mwenyekiti wa Jukwaa wa  Wahariri   Tanzania, Deodatus Balile amesema kuwa Wahariri  wameridhishwa na huduma za Ubingwa na Ubingwa bobezi zikiwemo za upandikizaji Uloto kwa watoto wenye Sikoseli na Upandikizaji Figo, huduma  ambazo hapo awali Watanzania walilazimika kwenda kuzifuata nje ya nchi kwa gharama kubwa.

"Tunaipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya, na tunawapongeza wataalam wa BMH kwa kazi kubwa wanazozifanya, hii ni kazi ya kitume,” amesema Balile.

Aliongeza kuwa Serikali iendelee kuweka mkazo wa Bima ya Afya kwa wote, itasaidia makundi yote katika jamii kuwa na uhakika wa kupata huduma za Afya hususani matibabu ya magonjwa yanayosumbua na yenye gharama kubwa za matibabu .

Ujio wa ujumbe wa wahariri wa vyombo vya habari kutembelea BMH ni muendelezo wa kuunga mkono kampeni ya kuchangia mfuko wa kuchangia matibabu ya figo na uloto unaoshirikisha wadau na makundi mbalimbali kwenye jamii.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dkt. Abdallah Baja amewaomba wahariri wa vyombo vya habari kutumia kalamu zao kuhamasisha wadau mbalimbali kujitokeza kuchangia mfuko wa matibabu ya upandikizaji uloto na figo ili kuwasaidia wagonjwa wengi zaidi kupata huduma .

Dkt. Baja ameongeza kuwa mchango wa vyombo vya habari ni muhimu Katika kufanikisha harambee ya mfuko wa matibabu kwa kuwa vina uwezo mkubwa wa kufikisha ujumbe kwa jamii na kuwahamasisha wadau mbalimbali kushiriki katika kusaidia wagonjwa wenye uhitaji.

“Tunawaomba Wahariri wa vyombo vya habari kuwa chachu katika kuhamasisha wadau mbalimbali kuchangia mfuko huu. Tunahitaji kuona wagonjwa wengi zaidi wakinufaika na huduma za upandikizaji uloto na figo ambazo sasa zinapatikanika hapa nchini hususan Hospitali ya Benjamin Mkapa, ” amesema Dkt. Baja.