WAZIRI WA AFYA MHE MOHAMED MCHENGERWA AZINDUA BODI YA PILI YA WADHAMINI YA BMH, AUNGA MKONO OMBI LA BMH KUWA HOSPITALI YA TAIFA

Published: Apr 24, 2026
WAZIRI WA AFYA MHE MOHAMED MCHENGERWA AZINDUA BODI YA PILI YA WADHAMINI YA BMH, AUNGA MKONO OMBI LA BMH KUWA HOSPITALI YA TAIFA cover image

Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA - APRILI 22, 2026

 

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb.) amesema kuwa anaunga mkono ombi la Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kupandishwa hadhi kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda na kuwa Hospitali ya Taifa.

 

 

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo wakati akizindua Bodi ya pili ya Wadhamini ya BMH ambapo amesisitiza kuwa amelibeba ombi hilo la kuwa Hospitali ya Taifa na kila atakapopata nafasi ya kuonana na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atamkumbushia ombi hilo.

 

 

"BMH ndio kioo cha Dodoma, ndio kioo cha Taifa letu kwa kuwa hapa Dodoma ndio Makao Makuu ya Taifa letu, BMH ina huduma bora zenye hadhi ya Kitaifa na Kimataifa, mazingira safi, uongozi na watumishi wake wana dhamira ya dhati ya kuwa na hadhi ya Taifa;  nimesikia malalamiko mengi katika Sekta ya Afya lakini Sijasikia malalamiko yanayoihusu BMH, pongezi kwa Viongozi na Wafanyakazi" alisisitiza Mhe. Mchengerwa.

 

 

Aliongeza kuwa hatua hiyo itaambatana na ongezeko la Watumishi, Vifaa Tiba, miundombinu na huduma mpya za kisasa za teknolojia ya leo huku akisisitiza kuwa Serikali inataka huduma zote za Kibingwa Bobezi zifanyike na kupatikana Dodoma BMH kama ilivyokuwa dhamira ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere wakati anaamua Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.

 

 

Mhe. Mchengerwa aliwamwagia sifa Wajumbe wa Bodi mpya ya Wadhamini ya BMH kuwa ni watu wenye weledi na uzoefu mkubwa katika sekta ya Afya nchini na kuwataka kuhakikisha wanaisimamia na kuifikisha mbali BMH, kukamilisha miradi yote inayoendelea kutekelezwa, kuanzisha miradi mipya na huduma mpya kadhalika na kuifanya BMH kuwa kinara wa huduma ya Utalii Tiba nchini.

 

 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo Prof. Edward Hoseah amemuomba Mhe. Waziri Mchengerwa kusaidia BMH kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi, upungufu wa magari kwa ajili ya kutolea huduma na kusaidia BMH iweze kulipwa  madeni ya jumla ya shilingi 14.39 Bil kutoka kwa Taasisi na Wadau mbalimbali waliohudumiwa na BMH.

 

 

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa BMH, imefanikiwa kuwa na huduma 20 za Ubingwa na 17 za Ubingwa Bobezi  (Ubingwa wa Juu).

 

 

"Huduma nyingi kati ya hizo zimeanza ndani ya kipindi cha uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tunamshukuru kwa kutoa fedha za kugharamia baadhi ya matibabu kama upandikizaji uloto kwa Watoto wenye ugonjwa wa Selimundu na Upandikizaji Figo" alisisitiza Prof. Makubi