WAZIRI KOMBO ATETA NA MKURUGENZI MTENDAJI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
DAR ES SALAAM - FEB 27, 2026
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa ya jijini Dodoma, Prof. Abel kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha sekta ya afya nchini kwa kuwashirikisha wadau wa ndani na nje ya nchi pamoja na mashirika ya kikanda na kimataifa.
Wakati wa mazungumzo yao yaliyofanyika Februari 27, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam, Prof Makubi alimshukuru Waziri Kombo kwa ushirikiano mkubwa wanaopata kutoka Wizarani wa kuwashirikisha wadau hususan wale wa nje ya nchi katika kuchangia maendeleo ya sekta ya afya nchini.
Kadhalika alimweleza Waziri Kombo kuwa, pamoja na jitihada hizo, Hospitali hiyo bado inahitaji kuungwa mkono hususan katika utoaji huduma za kibingwa kama upandikizaji figo na uloto ambazo matibabu yake ni ya gharama za juu.
Aliongeza kusema, mpango wa Hospitali ya Benjamin Mkapa wa kuwa na Kituo cha Umahiri cha magonjwa ya figo na upandikizaji figo katika ukanda wa Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara unaendelea vizuri ambapo ujenzi wa Kituo hicho kitakachogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 44.9 hadi kukamilika kwake unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari 2027 kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Shirika la Tiba la TOKUSHUKAI kutoka Japan.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaimarisha huduma za upandikizaji figo nchini, kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya, kufanya tafiti na kupunguza gharama lwa wagonjwa wanaolazimika kusafiri nje ya nchi kufuata huduma hizo.
Pia amesema, Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa imeendelea kutoa huduma za upandikizaji figo na upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa Selimundu (Sickle Cell) ambapo hadi sasa wagonjwa 56 wamepandikizwa figo kwa mafanikio na wagonjwa 26 wa Selimundu wote wakiwa watoto wamepandikizwa uloto na kupona.
Kwa upande wake, Mhe. Waziri Kombo alipongeza jitihada na kazi kubwa inayofanywa na Hospitali hiyo na kwamba yupo tayari kushirikiana nao ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma nzuri za matibabu hapa hapa nchini.