WASHIRIKI WA MISS WORLD TANZANIA 2026 WATEMBELEA BMH, WAPONGEZA UTOAJI HUDUMA

Published: Apr 15, 2026
WASHIRIKI WA MISS WORLD TANZANIA 2026 WATEMBELEA BMH, WAPONGEZA UTOAJI HUDUMA cover image

Na Gladys Lukindo, Dodoma Aprili 13

 

Washiriki 20 waliongia fainali ili kumpata mshiriki atakayeiwakilisha Tanzania katika mashindano ya urembo ya Dunia (Miss World) leo wametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), wakipongeza viwango vya utoaji huduma bora za Afya.

 

Mratibu wa mashindano hayo, Ndg.Mustapher Hassanali, amepongeza huduma za Hospitali ya Benjamin Mkapa.

 

" Kuna huduma ambazo zamani tulizipata nje ya nchi tu, lakini sasa tunazipata hapa hapa nchini katika Hospitali hii ya Benjamin Mkapa," amesema Ndg. Hassanali.

 

Bi Saraphina Kiyosaki, mmoja wa washiriki, amesema katika ziara ya BMH wameshuhudia uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali.

 

Mshiriki mwingine, Bi Jacqueline Nyabisi, amesema kama ilivyo kaulimbiu ya mashindano hayo, "Beauty with purpose," watatumia ushiriki wao wa Miss World kuhamasisha jamii kuchangia matibabu ya upandikizaji uloto na figo, ambayo BMH wanaendesha harambee kwa ajili ya kukusanya shilingi Bil. 7 kwa ajili ya kugharamia matibabu ya wanaoumwa magonjwa hayo ya Selimyndu na Figo.

 

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Ndg Teophory Mbilinyi, ameishukuru Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuchagua Hospitali ya Benjamin Mkapa kama sehemu mojawapo ya kutembelea.

 

"Washiriki wa Miss World ni jukwaa ambalo litaenda kututangaza kwa jamii na kusaidia kutangaza tiba utalii kwa nchi nyingine," amesema Ndg. Mbilinyi.