WALIMU WAKUU MANISPAA YA MOROGORO WACHANGIA FEDHA KUWEZESHA UPANDIKIZAJI ULOTO NA FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA

Published: Jul 04, 2026
WALIMU WAKUU MANISPAA YA MOROGORO WACHANGIA FEDHA KUWEZESHA UPANDIKIZAJI ULOTO NA FIGO KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA cover image

Na Jeremia Mwakyoma, Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - MEI 21, 2026

Umoja wa Walimu Wakuu Wanawake wa shule za msingi Manispaa ya  Morogoro (Solidarity Group) wamechangia Fedha jumla ya shilingi 210,000/= kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kama sehemu ya mchango wao kwenye mfuko maalumu wa kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Selimundu (Cickle Cell) na upandikizaji Figo kwa Watanzania wenye uhitaji (BMH Organ Transplant Fund).

Umoja huo wa Walimu Wakuu Manispaa ya Morogoro leo wametembelea BMH kujionea huduma ambapo walitumia ziara hiyo kukabidhi mchango wao wakisema umelenga kusaidia Watoto wenye Selimundu.


Akiongea na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH,  Mwenyekiti wa Umoja huo wa walimu Mwl. Blandina Joseph Mahai  amesema kuwa walimu wamefurahishwa na viwango vya huduma walivyoviona BMH, na wameshawishika na jitihada za Hospitali hiyo ya kushirikisha Wadau mbalimbali.kuunga mkono matibabu ya upandikizaji uloto na figo.

"Mchango huu wa jumla ya shilingi 210,000/= walimu tunauelekeza kwa watoto chini ya miaka 15 wanaosumbuliwa na tatizo la selimundu, tunaungana na Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia watoto wenye uhitaji na pia wenye uhitaji wa huduma za figo; aidha tumevutiwa na huduma zinavyotolewa na BMH, usafi, kumuona daktari ni rahisi, na watumishi wake ni wakarimu. Hakika tumejionea mazingira mazuri" alisisitiza Mwl. Mahai.


Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Ndugu Teophory Mbilinyi amewashukuru sana waalimu hao kwa moyo huo na kuwasihi kuendelea kutangaza mema waliyoyaona katika huduma zinazotolewa ndani ya BMH.

"Pamoja na kuwashukuru ndugu zetu walimu kwa moyo huu wa upendo mliouonesha, naomba nitumie fursa hii kutoa wito kwa watanzania wote, mwananchi mmoja mmoja, vikundi mbalimbali na wadau wengine kushiriki katika kuchangia mfuko huu wa kusaidia matibabu ya upandikizaji Uloto na Figo kwa kiwango chochote mtu atakachojaaliwa nacho hata kama ni kiasi kidogo kitakwenda kusaidia kuokoa maisha ya watanzania wenzetu wenye kuhitaji upandikizaji Ulotoa au Figo" alisisitiza Ndugu Mbilinyi.