MKUU WA MKOA WA MTWARA KANALI DONALD MSENGI AMEZINDUA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA BMH WILAYANI MASASI MKOANI MTWARA
Na Jeremia Mwakyoma
MASASI MTWARA - JUNI 3, 2026
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Kanali Donald Msengi leo amezindua rasmi kambi ya Madaktari Bingwa Bobezi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa inayofanyika Wilayani Masasi Mtwara huku akiwasisitiza Wananchi Wilayani humo na Wilaya za jirani kujitokeza kwa wingi kufanya uchunguzi na kupata matibabu.
"Kambi hii imesaidia kufikisha huduma za kibingwa kwa wananchi wa Masasi na Mkoa wa Mtwara kwa ujumla, imeunga mkono juhudi za Mhe Rais Samia za kufanya mapinduzi makubwa ya sekta ya Afya ili kuwapa wananchi huduma za ubingwa bobezi ikiwa ni pamoja na kujenga Hospitali za kisasa, kusomesha wataalamu na kuwa na vifaa tiba vya kisasa" alisisitiza Mhe. Msengi.
Mhe. Msengi aliwapongeza BMH, Benjamin Mkapa Foundation na SOTAC kwa kushirikiana kuwapelekea wana masasi huduma, akiongeza kuwa BMH ni Hospitali kubwa nchini yenye madaktari wenye ubingwa wa juu na teknolojia za kisasa jambo lililowezesha wananchi zaidi ya 385 kupatiwa matibabu hadi sasa na wengine kufanyiwa upasuaji kwenye magari maalumu yenye teknolojia za vyumba vya upasuaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Upasuaji wa BMH Dkt. Henry Humba akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa BMH pamoja na kutoa huduma za ubobezi ina jukumu la kuwapelekea wananchi huduma hizo kwenye maeneo ya vijijini na Wilaya ambazo huduma za upasuaji ni haba.
Tumeshapeleka kambi za upasuaji kwenye takribani mikoa 7, nje ya nchi kama Burundi na Comoro na kwa sasa tunajiandaa kwenda Malawi hivi karibuni; kwa kushirikiana na SOTAC tuna magari na vifaa vinavyotuwezesha kufika kwenye maeneo mbalimbali hadi ya vijijini kupeleka huduma
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Benjamin Mkapa Foundation Dkt. Ellen Senkoro ambao wameshirikiana na BMH kupeleka huduma Wilayani Masasi amesema kuwa taasisi yake inashirikiana na Serikali kwa muda mrefu kupeleka huduma za Afya hususani maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi.
Dkt. Senkoro ameahidi kuendeleza ushirikiano na BMH yenye mabingwa wabobezi wa kutosha katika kuendelea kuandaa kambi za matibabu ili kuwafikia wananchi wengi zaidi waliopo maeneo ambayo yana uhitaji wa huduma za ubobezi.