Zingatia matumizi sahihi ya dawa
Na Ludovick Kazoka
Picha: Jeremiah Mbwambo na Gladys Lukindo
Dodoma - Septemba 25, 2025
Wakati Dunia ikiazimisha Siku ya Wafamasia leo, Hospitali ya Benjamin Mkapa imewataka wateja wake kuzingatia matumizi sahihi ya dawa wanavyoelekeza na wafamasia Hospitalini hapo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Prof Abel Makubi, akisema matumizi holela ya dawa yanaweza kusababisha matatizo ya kiafya.
"Ukishapewa dawa, una haki ya kumuulizia mfamasia jinsi ya kuzitumia ili usiji-overdose," amesema Mkurugenzi Mtendaji.
Prof Makubi amesema ni muhimu pia fursa hiyo kuwashauri wateja kuhakikisha wanazijua dawa wanazoenda kuzitumia.
"Hakikisha unakuwa unazijua dawa unazokwenda kuzitumia na usisite kumuuliza mfamasia zinapokuchanganya, uliza ili uzitumie kiusahihi," ameongeza Prof Makubi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Famasi, Bi Emiliana Bernado, amesema kuwa famasi zote tatu za BMH wamejipanga kwa ajili ya ugawaji dawa na kutoa maelekezo sahihi ya dawa.
"Unapopewa dawa ni haki yako kuuliza matumizi ya dawa hizo," amesema Bi Emiliana.
Ndugu Samuel Mbogo, mmoja wa wateja, alitaka kujua anapopewa dawa nyingi anapaswa kuzitumia zote kwa wakati mmoja au anaruhusiwa kusimama.
"Kuna wakati unajikuta umepewa lundo la dawa, sasa unaweza ukaacha kuzitumia nyingine au unapaswa kuzitumia zote" amesema.