WAKURUGENZI WA ORCI na BMH WATEMBELEANA NA KUSHAURIANA JUU YA HATUA ZA UJENZI WA KITUO CHA UMAHIRI CHA SARATANI KATIKA HOSPİTALI YA BENJAMIN MKAPA
Na Jeremia Mwakyoma, Jeremia Mbwambo
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - JULAI 6, 2026
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) , Dkt. Diwani Msemo leo ametembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kituo cha umahiri cha matibabu na mafunzo ya saratani na kufanya mazungumzo na mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi juu ya kukuza zaidi ushirikiano baina ya taasisi hizo.
Baada ya kutembelea ujenzi wa kituo hicho, Dkt. Msemo amepongeza kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa kituo hicho na kuahidi ushirikiano wa karibu kwa BMH katika kuhakikisha kituo hiko kinaanza kazi ya kutoa matibabu ya ubingwa ya saratani, mafunzo na tafiti za afya juu ya Saratani mara tu kitakapokamilika.
"Naipongeza na kuishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza ujenzi wa kituo hiki cha umahiri cha Saratani ambacho kitakuwa miongoni mwa vituo vikubwa hapa nchini vya huduma za kibingwa za saratani, mafunzo na tafiti, kituo hiki kitasaidia sana kupunguza mzigo mkubwa wa wagonjwa wengi hapa nchini kutegemea ORCI katika huduma za matibabu ya Saratani" alisisitiza Dkt. Msemo.
Katika ukaguzi wa ujenzi wa mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi alitumia nafasi hiyo kumuagiza Mkandarasi wa mradi huo Kampuni ya Mohamed Builders na Msimamizi Mshauri wa mradi TBA kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa ili uanze kutoa huduma kwa wananchi huku akiishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo.
Mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 71 na unatarajiwa kukamilishwa mwishoni mwa mwaka huu 2026 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 32.