WANANCHI ZAIDI YA MILIONI NNE (4) WAFIKIWA NA HUDUMA ZA UBINGWA BOBEZI MWAKA 2025/26

Published: May 14, 2026
WANANCHI ZAIDI YA MILIONI NNE (4) WAFIKIWA NA HUDUMA ZA UBINGWA BOBEZI MWAKA 2025/26 cover image

Na Hassan Kimweri, WAF - Dodoma 

 

 

Wagonjwa zaidi ya milioni 4 wamefikiwa na huduma za ubingwa bobezi nchini katika mwaka wa fedha 2025/26 hatua inayodhihirisha kuimarika kwa sekta ya afya na kupanuka kwa huduma za kibingwa nchini chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

 

Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hayo leo Mei 11, 2026 wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2026/27 katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Spika wa Bunge Mhe. Mussa Azan Zungu. "Jumla ya wagonjwa milioni 4,202,137 walipata huduma za ubingwa bobezi katika hospitali mbalimbali huku huduma maalum zikiwemo IVF, upandikizaji wa figo, vifaa vya usikivu, puto tumboni, huduma za meno, upasuaji wa goti au nyonga pamoja na upandikizaji wa uloto zikisaidia kuokoa takribani Shilingi bilioni 3.67 ambazo zingetumika kwa matibabu nje ya nchi," amesema Waziri Mchengerwa

 

 

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia waliendelea kutoa huduma katika halmashauri mbalimbali ambapo wagonjwa elfu 55,300 walihudumiwa katika halmashauri mia 184 nchini, huku wataalam elfu 5,585 wakijengewa uwezo kupitia huduma hizo maalum za kibingwa.

 

 

“Serikali inaendelea kusogeza huduma za ubingwa karibu na wananchi ili kupunguza gharama za matibabu na kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya nchini,” amesema Waziri wa Afya. Katika kuimarisha huduma za mkoba, Waziri Mchengerwa amesema wagonjwa elfu 77,118 walifikiwa na huduma hizo huku wagonjwa elfu 3,018 wakihudumiwa kupitia tiba utalii na wagonjwa elfu 4,363 wakipatiwa huduma za matibabu nje ya nchi. Kwa upande wa uuguzi na ukunga, Waziri Mchengerwa amesema sekta hiyo ambayo hutoa takribani asilimia 80 ya huduma za afya imeendelea kuimarishwa kupitia mafunzo ya wakunga elfu 1,850 na kufanya jumla ya waliopata mafunzo kufikia elfu 9,093.