KAMATI YA KUDUMU YA BAJETI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAIPONGEZA SERIKALI KWA UWEKEZAJI BMH

Published: Aug 26, 2026
KAMATI YA KUDUMU YA BAJETI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAIPONGEZA SERIKALI KWA UWEKEZAJI BMH cover image

Na Jeremia Mwakyoma, Jeremiah Mbwambo
PICHA NA GLADYS LUKINDO - AGOSTI 26, 2026

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Makamu Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Mariam Said Hamis amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa uliofanyika BMH na kuiwezesha kutoa huduma 20 za ubingwa na 17 za ubingwa bobezi katika kiwango cha ubora na mazingira mazuri.

 

"Zamani magonjwa mengi makubwa wananchi walikuwa wanalazimika kufuata mbali matibabu yake kwa gharama kubwa kwenye nchi za Asia, Ulaya na Amerika, lakini kwa sasa matibabu mengi yanapatikana hapa nchini ikiwemo BMH, tumeshuhudia madaktari na Wauguzi werevu,wenye moyo wa kuwapokea na kuwahudumia wagonjwa kwa ukarimu, mazingira ya hospitali na hali ya juu ya usafi unaweza ukafikiri uko hotelini badala ya hospitali. Alisisitiza Mhe. Hamis.

 

Makamu Mwenyekiti Hamis aliongeza kuwa baadhi ya huduma za kibobezi zinazotolewa na BMH kama upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Sickle Cell zinatoa faraja kwa nchi yetu na nchi za jirani na zinawezesha kuvuta Rais wa mataifa mengine kama Congo DRC na Burundi kuleta wagonjwa wao kuja kutibiwa BMH.

 

Ameongeza kuwa kamati yao inatarajia wakati wowote BMH itaanza kutoa matibabu ya ubingwa wa juu ya Saratani ikiwemo tiba mionzi mara tu baada ya mradi wa kituo cha umahiri cha matibabu na mafunzo ya saratani kitakapokamilika; Aidha, amesisitiza kupitia ushirikiano uliopo kati ya mfuko wa bima ya Afya ya Zanzibar na Bima ya Afya ya Taifa wanatarajia wananchi kutoka Zanzibar watakuwa wanapata huduma za Afya katika Hospitali za Bara kupitia utaratibu huo wa Bima.

 

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Dkt. Abdallah Baja amesema BMH inapenda ushirikiano na Zanzibar ikiwemo kubadilishana utaalamu na uzoefu, programu za kubadilishana wataaalamu kwa ajili ya kutoa matibabu na kuwakaribisha wananchi kutoka Zanzibar kuja kupata matibabu BMH ikizingatiwa BMH ina uwezo mkubwa.

 

Nae Kaimu Mkuu wa Mawasiliano na Mahusiano wa BMH Jeremiah Mbwambo amebainisha kuwa kwa sasa BMH inahudumia wagonjwa wa nje takribani 1200 kwa siku, pia inafundisha na kusaidia kuzalisha wataalamu wa afya na kufanya tafiti zinazohusu masuala ya Afya.