WAZIRI MKUU AWEZESHA UWT KUCHANGISHA BIL 2.4 KUOKOA MAISHA YA WATOTO BMH
Na. Jeremiah Mbwambo na Jeremia Mwakyoma
Picha: Gladys Lukindo
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba(Mb), ametoa wito kwa Watanzania, taasisi za umma na binafsi, mashirika pamoja na wadau wa maendeleo kuungana na Serikali katika kuwezesha matibabu ya upandikizaji wa figo na uloto kwa wananchi wasiokuwa na uwezo, ili kuokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji huduma hizo za kibingwa.
Akizungumza katika hafla ya Okoa Maisha Gala iliyoandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kushirikiana na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), iliyofanyika jana Julai 16, 2026, katika Ukumbi wa Mabele Hall, jijini Dodoma, Dkt. Nchemba amesema kushiriki katika kuwasaidia wagonjwa ni tendo la utu, huruma na uzalendo.
"Tunachokifanya leo ni kurejesha matumaini kwa wagonjwa na familia zao. Kila anayeguswa na jambo hili aendelee kushiriki ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma hizi muhimu, akihitimisha changizo alitoa taarifa ya ahadi na pesa taslimu katika usiku huo ni shilingi Bilioni 2.4" alisema.
Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, kuongeza vifaa tiba na kuimarisha huduma za kibingwa ili Watanzania wengi zaidi wapate matibabu ya kiwango cha juu hapa nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisema Serikali itaendelea kuimarisha huduma za kibingwa kupitia uwekezaji katika miundombinu ya afya, vifaa tiba na rasilimali watu, huku akihamasisha wadau kuendelea kuchangia Mfuko wa Matibabu ya Upandikizaji wa Figo na Uloto.
.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa, Profesa Abel Makubi, alisema hospitali hiyo imefanikiwa kufanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 58 na upandikizaji wa uloto kwa watoto 31 wenye ugonjwa wa selimundu.
.
Amesema kuwa kampeni ya Okoa Maisha inalenga kukusanya shilingi bilioni saba zitakazotumika kusaidia matibabu ya wagonjwa wenye uhitaji pamoja na kupanua miundombinu ya huduma za upandikizaji wa figo na uloto.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia matibabu ya wagonjwa pamoja na kuboresha miundombinu ya huduma hizo nchini.