WAZIRI MKUU: USHUHUDA WA FAMILIA ZILIZONUFAIKA NA MATIBABU YA BMH UMENIGUSA,MNASTAHILI PONGEZI

Published: Jul 20, 2026
WAZIRI MKUU: USHUHUDA WA FAMILIA ZILIZONUFAIKA NA MATIBABU YA BMH UMENIGUSA,MNASTAHILI PONGEZI cover image

Na Jeremia Mbwambo na Jeremia Mwakyoma Picha na Gladys Lukindo 

DODOMA - JULAI 16, 2026

 

WAZIRI Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba amesema ushuhuda alioupata kutoka kwa familia zilizonufaika na huduma za upandikizaji wa uloto katika Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) umemthibitishia kuwa uwekezaji wa Serikali katika sekta ya afya umeanza kuokoa maisha ya Watanzania na kuondoa utegemezi wa kutibiwa nje ya nchi.

 

Dk. Nchemba alisema katika ziara na mikutano mbalimbali anayoifanya amekutana na familia zilizowahi kupata huduma za upandikizaji wa uloto hapo BMH, ambazo zimetoa ushuhuda wa namna huduma hizo zilivyowarejeshea matumaini baada ya wagonjwa wao kupona na kurejea kwenye maisha yao ya kawaida na majukumu yao.

 

Dkt. Nchemba aliyasema hayo wakati wa hafla ya kuchangia fedha kwenye mfuko wa kusaidia matibabu ya upandikizaji wa Uloto na upandikizaji Figo BMH ambapo alisisitiza kuwa jambo hilo linaonesha kuwa mafanikio yayopatikana katika hospitali hiyo si ya kawaida, bali ni matokeo ya uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kuboresha huduma za afya.

 

"Jambo tunalolizungumza leo si la kishabiki, ni la maisha. Linahitaji moyo wa kitaifa kwa sababu huduma hizi zimeokoa maisha ya watu na wakati huohuo zimeokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwapeleka wagonjwa nje ya nchi," alisema.

 

Alisema si mataifa mengi barani Afrika yenye uwezo wa kutoa huduma za upandikizaji wa figo na uloto kama zinazotolewa na BMH, jambo linaloifanya Tanzania kuendelea kujijengea heshima katika sekta ya afya.

 

Dk. Nchemba aliipongeza BMH kwa mafanikio hayo makubwa, akisema hospitali hiyo imekuwa mfano wa uwekezaji wenye matokeo chanya kwa wananchi. Alisema wagonjwa kutoka mikoa ya Morogoro, Iringa, Manyara, Tabora, Kigoma, Tanga, Singida pamoja na maeneo mengine ya nchini wamekuwa wakifika BMH kupata huduma hizo za kibingwa, hali inayoifanya hospitali hiyo kuwa kituo muhimu cha rufaa kwa matibabu ya figo na uloto. Alisema Serikali itaendelea kuwa bega kwa bega na BMH ili kuhakikisha huduma hizo zinaimarishwa zaidi na Watanzania wengi wanaohitaji matibabu hayo wanapata fursa ya kuhudumiwa nchini.

 

Dk. Nchemba aliupongeza Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kwa kuanzisha kampeni ya uchangishaji fedha kwa ajili ya Mfuko wa Upandikizaji wa Figo na Uloto, akisema wamefanya jambo kubwa ambalo hata BMH haikutarajia. Alisema hatua hiyo inaonyesha uzalendo na utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Alisema tayari kampeni hiyo imefanikiwa kufikia asilimia 70 ya lengo la ukusanyaji wa fedha, hatua inayoonyesha mwitikio mkubwa wa wadau na wananchi.

 

Dk. Nchemba alisema fedha zitakazopatikana katika hafla hiyo zitatumika kusaidia watoto na watanzania wenye uhitaji wa matibabu ya upandikizaji Uloto na Figo na pia kusaidia upande wa vifaa tiba vya huduma za upandikizaji wa figo na uloto, jambo litakaloongeza uwezo wa hospitali kuhudumia wagonjwa wengi zaidi. Dkt. Nchemba aliwapongeza watu wote, taasisi na makampuni yaliyotoa michango kwa mfuko huo na kwamba Serikali inatambua mchango na uzalendo wao wa kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania. Aidha, alitoa wito kwa taasisi nyingine za umma, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi kuendelea kujitokeza kuchangia mfuko huo ili wagonjwa wengi zaidi wanaohitaji upandikizaji wa figo na uloto wapate matibabu kwa wakati na kurejeshewa matumaini ya maisha.