Mwanzo / Huduma Zetu / PROF. MAKUBI AWASISITIZA WAJUMBE WA MENEJIMENT YA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUFANYA USIMAMIZI SHIRIKISHI

PROF. MAKUBI AWASISITIZA WAJUMBE WA MENEJIMENT YA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUFANYA USIMAMIZI SHIRIKISHI

Published on April 06, 2025

Article cover image

Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Ludovick Kazoka
DODOMA-April 5, 2025

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof. Abel Makubi amewataka Wajumbe wote wa Menejimenti ya hospitali hiyo kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika zoezi la usimamizi shirikishi  wa utoaji huduma za Afya na uendeshaji wa Hospitali. 

Prof Makubi ametoa maelekezo hayo leo wakati wa ziara ya ukaguzi na ufuatiliaji wa hali ya utoaji huduma Hospitali hapo ambayo ni sehemu ya usimamizi shirikishi aliyoifanya akiwa ameambatana na wajumbe wa Menejimenti ya BMH. 

"Zoezi la usimamizi shirikishi ni la lazima kufanyika na ni utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Afya ambayo baada ya kuona utoaji wa huduma unalegalega nyakati za mwisho wa wiki (week end) na nyakati za baada ya masaa ya kazi wakatoa Muongozo wa kuzitaka Menejimenti za Hospitali kuweka utaratibu wa kufanya usimamizi shirikishi ili kuboredha utoaji huduma, kubaini changamoto zilizopo na kuzitafutia ufumbuzi kwa lengo la kuboresha huduma" Alisisitiza Prof. Makubi 

Alibainisha kuwa hapo awali zoezi hilo lilikuwa likifanyika lakini hapo kwa muda kama wa miezi miwili zoezi hilo limesimama bila kufanyika na kuongeza kuwa hata wakati likifanyika matokeo yake yalikuwa hayakidhi matarajio yote yaliyohitajika hivyo uongozi wa BMH ukaamua kuja na mkakati wa kuboresha zoezi hilo la usimamizi shirikishi na ukaguzi wa utoaji huduma na uendeshaji. 

"Usimamizi shirikishi unasaidia kuleta uwajibikaji wa pamoja kati ya Menejimenti nzima ya Hospitali na Watumishi wengine na kwa kufanya ziara za ukaguzi kwenye maeneo ya kutolea huduma unasaidia kupata hali halisi ya huduma zinazotolewa, changamoto zilizopo kwenye maeneo ya kutolea huduma, lakini pia inasaidia kuonana na Wagonjwa  na Ndugu za Wagonjwa na kupata mrejesho kutoka kwao juu ya huduma wanazopatiwa na Hospitali. 

Nae Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Bw. Theophory Mbilinyi amesisitiza kuwa zoezi hilo la usimamizi shirikishi limejumuisha Wajumbe wenye taaluma na Idara mbalimbali ikiwemo TEHAMA, Ufundi, Sheria, Manunuzi, Fedha, Wataalamu wa Afya na Tiba ili kuweza kutatua changamoto za aina yoyote zitakazobainika. 

"Utaratibu wa kuwa na idara na Wataalamu tofautitofauti unatupa uwezo wa kukabili na kutatua changamoto tunazozibaini katika utoaji huduma kwa kuwa Wataalamu wenye ujuzi wanakuwepo maeneo yote tunayopita kufanya  ukaguzi" alisisitiza Bw. Mbilinyi. 

Nae Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Ufundi hapo BMH Bw. Frank Asenga amesema kuwa anatambua kitengo cha ufundi kina idara nyingi za muhimu zenye kuboresha huduma za hospitali kama Biomedical Engineering, Kitengo cha umeme, kitengo cha maji na miundombinu mingine yote ya taasisi na kuahidi kusimamia maeneo yote hayo kwa ufanisi ili kutatua changamoto mbalimbali zilizopo na zitakazojitokeza wakati wowote. 

Bw. Sadick Sangawe ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha manunuzi wa BMH pamoja na kupongeza mfumo wa usimamizi shirikishi, nae amebainisha kuwa kitengo chake kinaingia karibu kwenye idara zote zilizopo BMH hivyo ameahidi kuongeza ushirikiano na idara zote ili kurahisisha mchakato wa manunuzi kwa kuhakikisha wanapata wazabuni wazuri, kupata vifaa vyenye ubora kwa gharama nafuu na kwa wakati. 

Bw. Sangawe amesema kuwa wameboresha usimamizi wa Ghala la vifaa vya ufundi na watahakikisha kuwa vifaa vyote muhimu kwa ajili ya kufanyia matengenezo kinga ya vifaa tiba na miundombinu mbalimbali vinapatikana kwa urahisi na kwa haraka ili uhakikisha vifaa na miundombinu yote inafanya kazi kwa ufanisi wakati wote na ile yenye hitilafu kurekebishwa kwa haraka na huduma kuwa bora wakati wote. 

Zoezi la Usimamizi shirikishi lilihusisha ukaguzi wa Mtambo wa Kuzalisha hewa tiba, Karakana ya kukarabati Vifaa tiba na vya kutolea huduma vilivyoharibika na kuweka mpango wa kushughulikia maeneo yale yaliyobainika kuwa na ubovu na changamoto mbalimbali. 

Maeneo mengine yaliyokaguliwa ni miundombinu muhimu ya huduma za Afya, usafi wa mazingira na usafi wa Hospitali na maeneo yote ya kutolea matibabu na huduma kwa wananchi, Wodi za kulaza Wagonjwa, kukagua wasimamizi na watoa huduma kwenye maeneo yote ya Hospitali, kuzungumza na Wagonjwa wanaopata huduma na waliolazwa Hospitalini hapo kwa ajili ya kupata maoni yao kuhusiana na huduma wanazopewa na kufanya ufuatiliaji kwenye mtandao/mfumo wa TEHAMA wa Hospitali kuona namna huduma zinavyotolewa kwa Wagonjwa.