PROF MAKUBI rasmi Benjamin Mkapa Hospital
Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Prof Abel Makubi leo ameripoti rasmi Hospitali hii ya Rufaa iliyoko Makao Makuu ya nchi Dodoma.
Prof Makubi anachukua nafasi hiyo kufuatia uteuzi uliofanywa Mhe Rais Samia Suluhu Hassan, tarehe 4 Juni baada ya Dkt Alphonce Chandika kumaliza muda wake.
Akiongea baada ya kukabidhiwa ofisi, Prof Makubi, amewataka watumishi wa BMH kulipeleka kwa kasi lengo la kuifanya BMH kuwa Hospitali ya Taifa na kumshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini tena kuwatumikia Wananchi .
"Lengo sio tu kuifanya BMH iwe Hospitali ya Taifa bali iwe ya kimataifa, na ya kisasa na ubora zaidi, hivyo tufanye kazi kwa umoja, ushirikiano na kujituma," amesema Mkurugenzi Mtendaji mpya wa BMH.
Kabla ya uteuzi huo, Prof Makubi, alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa (MOI) na amewashukuru sana watumishi na menejimenti ya huko kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati akifanya nao kazi pamoja.
Prof Makubi ametumia fursa hiyo kumpongeza Mkurugenzi Mtendaji anayemaliza muda wake Dkt Alphonce Chandika na kusema ataendeleza yale yote mazuri aliyoyafanya BMH.
"Naomba nikupongeze Dkt Chandika ulipokuja hapa BMH kulikuwa na sintofahamu, lakini umefanya mageuzi makubwa katika Hospitali hii," amesema Prof Makubi.
Kwa upande wake, Dkt Chandika, amewashukuru wafanyakazi wote wa BMH kwa kumapatia ushirikiano mkubwa wakati akitekeleza majukumu yake.
"Nawashukuru watumishi wenzangu kwa ushirikiano mkubwa mlionipatia wakati natakeleza majukumu yangu na hivyo kufikisha hapa BMH," alihitimisha Dkt. Chandika.