TANGAZO KWA UMMA:  OSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUTOA HUDUMA ZA AFYA ZA UBINGWA NA UBINGWA BOBEZI NCHINI MALAWI KUPITIA KAMBI ZA HUDUMA ZA AFYA

Published: Sep 27, 2026
TANGAZO KWA UMMA:  OSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KUTOA HUDUMA ZA AFYA ZA UBINGWA NA UBINGWA BOBEZI NCHINI MALAWI KUPITIA KAMBI ZA HUDUMA ZA AFYA cover image

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Tanzania, inayo furaha kuutaarifu umma kuhusu hatua muhimu katika kuimarisha huduma zake za afya kwa nchi za jirani. Hospitali itatoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kupitia kambi za huduma za afya nchini Malawi kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 9 Oktoba 2026, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kupanua upatikanaji wa huduma za afya za kiwango cha juu na kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika sekta ya afya Barani Afrika.

 

Kambi hizo za huduma za afya zitafanyika kwa ushirikiano na TPA, AZAM, MSD na SOTAC, pamoja na mamlaka husika za afya na hospitali nchini Malawi. Kambi ya kwanza itafanyika katika Hospitali ya Mzuzu Central kuanzia tarehe 28 Septemba hadi 2 Oktoba 2026, ikifuatiwa na kambi ya pili katika Hospitali ya Kamuzu Central kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026.

 

Timu ya wataalamu mbalimbali wa kada za afya kutoka BMH, wakiwemo wataalamu wa ubingwa na ubingwa bobezi, itatoa huduma za ushauri wa kitaalamu, uchunguzi wa kitabibu, uchunguzi wa awali, tathmini na baadhi ya huduma za matibabu katika maeneo yafuatayo:

  •        Upasuaji wa Mifupa na Viungo
  •        Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu pamoja na Mgongo
  •        Upasuaji wa Jumla
  •        Huduma za Magonjwa ya Moyo
  •        Huduma za Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo
  •        Uchunguzi na Tathmini kwa ajili ya Upandikizaji wa Figo
  •        Uchunguzi na Tathmini kwa ajili ya Upandikizaji wa Uloto

Mpango huu ni hatua muhimu katika jitihada za BMH za kupanua huduma za afya za ubingwa na ubingwa bobezi nje ya Tanzania. Aidha, unatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano wa kitaalamu, kubadilishana ujuzi na uzoefu, kuimarisha mifumo ya rufaa ya kikanda, pamoja na kujenga ushirikiano kati ya taasisi za afya za Tanzania na Malawi.

 

Kupitia mpango huu, BMH inalenga kuchangia katika lengo pana la kuongeza upatikanaji wa huduma za afya za kiwango cha juu barani Afrika, huku ikipunguza ulazima wa wagonjwa kusafiri nje ya bara hili kwa ajili ya kupata matibabu ya kibingwa.

 

Hivyo, BMH inawahimiza wananchi nchini Malawi wanaohitaji huduma hizi kufika katika kambi husika kwa ajili ya uchunguzi, ushauri wa kitaalamu, tathmini ya kitabibu na kupata matibabu stahiki au rufaa, kulingana na hali zao za kiafya.

 

Kwa pamoja, tunaendeleza upatikanaji wa huduma za afya bora, zenye ubora wa hali ya juu, za kibingwa na zinazowafikia wananchi barani Afrika.

 

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma

Hospitali ya Benjamin Mkapa

Dodoma, Tanzania