KLABU YA ROTARY KWA UKANDA WA NCHI YA TANZANIA NA UGANDA WAAHIDI USHIRIKIANO ZAIDI KWA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA
Na Jeremia Mwakyoma
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - FEB 16, 2026
Umoja wa Vilabu vya Rotary kwa ukanda wa nchi za Tanzania na Uganda wameahidi kuendeleza ushirikiano na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwa lengo la kuwezesha Jamii kupata huduma bora za Afya zikiwemo matibabu ya upandikizaji Uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa Sickle Cell na pia upandikizaji Figo.
Hayo yamebainishwa na Gavana wa Klabu za Rotary kwa ukanda wa nchi za Tanzania na Uganda Bi. Kristine Kawooya alipofanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa ambapo alipata fursa ya kujionea utoaji huduma za Afya kwenye idara ya upandikizaji Uloto na kuona upanuzi wa kituo cha upandikizaji figo.
"Tunaweza kuunganisha nguvu na tuko tayari kusaidiana na BMH, kushirikisha Wadau zaidi na Jamii ili kuwezesha huduma za upandikizaji Uloto kwa Watoto wenye Sickle Cell na matibabu ya upandikizaji Figo; Jamii ikiwezeshwa Taifa linakuwa limewezeshwa pia" alisisitiza Bi. Kawooya huku akitoa Rai kwa vyombo vya habari navyo kuunga mkono programu hizo kwa kuwa vinawafikia watu wengi zaidi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof Abel Makubi ameshukuru ufadhili wa Rotary Club wa kujenga Maabara Maalumu ya Mafunzo ya utoaji huduma za Afya (Skills Lab) ambayo imesaidia kuleta mapinduzi katika kuwapa mafunzo ya ujuzi watoa huduma na wanafunzi ambao watasaidia Taifa kwa muda mrefu.
Prof. Makubi aliongeza kuwa kwa sasa BMH inaendelea kuimarisha programu ya huduma za upandikizaji uloto ili kusaidia watoto wenye ugonjwa wa Sickle Cell, inaendelea kuimarisha Programu za upandikizaji Figo na Matibabu ya Saratani ambavyo vyote vinahitaji gharama lakini vinasaidia Watu wengi wenye magonjwa ya aina hiyo na kuwarejeshea tumaini lao katika Jamii.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi anaeshughulikia Mafunzo hapo BMH Dkt. Emiliana Myovela alitumia ziara hiyo kushukuru Klabu za Rotary kwa mchango wao wa kuwezesha mafunzo kwa Watoa huduma za Afya kupitia Maabara ya Mafunzo (Skills Lab) ya BMH ambapo jumla ya Wataalamu 269 Madaktari na Wauguzi wameweza kupata mafunzo mbalimbali yakiwemo ya upasuaji, dharura za ajali, huduma za Uzazi na ukunga ili kwenda kuboresha zaidi huduma wanazotoa kwa jamii kwenye maeneo mbalimbali ya nchi.
Nae rais wa Klabu ya Rotary ya Mwl. Nyerere ya Dodoma Dkt. Paul Nandire ametoa wito kwa Wana Dodoma kujiunga na Klabu za Rotary na kuanzisha Klabu za Rotary ikiwemo BMH kuwa na Klabu yake ya Rotary huku akibainisha kwa sasa kuna takribani Wanachama wa Klabu za Rotary 4000 na hivyo kusisitiza juu wa Watmdau wengi zaidi kujiunga.