KAMBI MAALUM YA MADAKTARI BINGWA WA MOYO KUTOKA BMH YAZINDULIWA MKOANI RUVUMA

Published: Nov 18, 2025
KAMBI MAALUM YA MADAKTARI BINGWA WA MOYO KUTOKA BMH YAZINDULIWA MKOANI RUVUMA cover image

Na Jeremia Mwakyoma

SONGEA, RUVUMA - NOVEMBA 17, 2025

Kambi Maalum ya Madaktari Bingwa Wabobezi wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto na Watu wazima kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inayofanyika Mjini Songeaย  Mkoani Ruvuma imefunguliwa Leo na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Brigadia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed.

Akifungua kambi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa na kuiendeleza Sekta ya Afya hapa nchini jambo linalowezesha kuwapelekea Wananchi huduma za Ubingwa na Ubingwa Bobezi karibu kwenye maeneo yao.

"Mhe. Rais ameweka msisitizo na kipaumbele cha kuhakikisha kambi hizi za matibabu zinafanyika kwenye Mikoa na Wilaya ili kuhakikisha zinawafikia wananchi walio wengi; aidha, matibabu haya ya Moyo na Elimu itakayotolewa ni vya muhimu kwani takwimu zinaonesha magonjwa ya Shinikizo la Damu na Moyo ni miongoni mwa magonjwa yanayowakabili Wananchi wengi, hivyo niwashukuru pia BMH kwa kutuletea huduma hizi" alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Kapenjama Ndile amebainisha kuwa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songea inapokea pia Wananchi wengi wa Mataifa jirani ikiwemo Malawi na Msumbiji.

"Hospitali hii ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma ndio Hospitali kubwa hapa Ruvuma, lakini kutokana na Ukaribu wake kijiografia na uwekezaji alioufanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Hospitali hii pia inapokea Wananchi wengiย  kutoka nchi za Malawi na Msumbiji nao wanakuja kutibiwa hapa, hivyo BMH mjiandae kupokea pia Wananchi wa nchi hizo na wengine watawafuata hadi Mkoani Dodoma kwa huduma zaidi" aliongeza Mhe. Ndile.

Nae Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Huduma Mkoba wa BMH Ndg. Rayhan Mbisso amebainisha kuwa BMH ina jukumu la kufikisha huduma zake za Ubingwa na Ubingwa wa Juu kwa Wananchi kwenye Mikoa kupitia Programu hii ya huduma Mkoba ambayo pia BMH inaitumia programu hiyo kuzijengea uwezo Hospitali za Mikoa na Wilaya.

"Madaktari Bingwa Wabobezi wa Magonjwa ya Moyo kwa Watoto na Watu Wazima watakuwepo hapa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Ruvuma kuanzia Leo hadi Ijumaaย  Novemba 21, 2025 wakitoa huduma za uchunguzi na matibabu, hivyo Wananchi mnashauriwa kutumia fursa hiyo ya kuja kupata huduma" alimalizia kwa kusisitiza Ndg. Mbisso.

Kwa upande wake Ndg. Evalisto Ngole Mkazi wa Manispaa ya Songea amesema kuwa mpango huu wa kambi za Matibabu unasaidia Wananchi wengi ambao hawana uwezo wa kusafiri kuzifuata huduma hizi za Ubingwa kwenye Hospitali kubwa zenye madaktari Bingwa Wabobezi kuzipata huduma hizo kwenye mikoa yao.