KAMBI YA MADAKTARI BINGWA NA BINGWA BOBEZI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA YAANZA WILAYANI IRAMBA MKOANI SINGIDA, WANANCHI WAITIKIA
Na Jeremia Mwakyoma
SINGIDA - FEB 24, 2026
Kambi ya Uchunguzi na Matibabu inayoendeshwa na Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imeanza rasmi Leo katika Hospitali ya Wilaya ya Iramba Mkoani Singida huku muitikio wa Wananchi ukiwa wa kuridhisha.
Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Huduma Mkoba wa BMH ambaye ndio kiongozi wa msafara Dkt. Emiliana Myovela amesema kuwa timu ya Madaktari Bingwa Bobezi kutoka BMH waliopo Singida inajumuisha matibabu ya Moyo kwa Watoto, kwa Watu wazima, Magonjwa ya ndani, Wakina mama na Uzazi, Mifupa, Upasuaji.
"Tutakuwa hapa Hospitali ya Wilaya ya Iramba (kiomboi) kuanzia Leo hadi Ijumaa Feb 27, 2026 tukitoa huduma ya uchunguzi na matibabu kwa Wananchi, tunashkuru mwitikio wao umekuwa mzuri waliposikia Benjamin Mkapa inakuja Iramba" alifafanua Dkt. Myovela.
Aliongeza kuwa BMH imeshafanya huduma mkoba (kambi za matibabu) katika nchi za Burundi, Comoro na sasa wanajiandaa kwenda Malawi; kwa upande wa mikoa hapa nchini ndani ya kipindi cha miezi sita wameshapeleka huduma Mkoani Ruvuma, Tabora, Singida na Dodoma yenyewe; tumekuja na magari maalumu yenye vyumba vya upasuaji na vifaa vya kisasa vya kufanyia matibabu.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick mara baada ya kutembelea kambi hiyo na kujionea utoaji huduma amepongeza teknolojia ya magari makubwa Maalumu ambayo yana vyumba vya Upasuaji na vifaa tiba vingine vya kutolea huduma.
Dkt. Ludovick ametoa wito kwa Wananchi wa Singida na Wilaya ya Iramba kutumia fursa hiyo kuja kupima Afya na kupata matibabu; amesema uzinduzi rasmi wa kambi hiyo utafanywa kesho na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego