MADAKTARI BINGWA WABOBEZI WA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA WAMEWEKA KAMBI MAALUM YA WIKI MOJA YA KUTOA MATIBABU WILAYANI PANGANI MKOANI TANGA
Pangani - Tanga
Timu ya madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa wameweka kambi ya wiki moja katika Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga kwa lengo la kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi.
Akizungumza mara baada ya kuwasili katika ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Bi.Lilian Marwa Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mafunzo na Huduma Mkoba kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa kambi hiyo ya matibabu itafanyika hadi Ijumaa Mei 8, 2026 na kuwa wataalamu hao wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanatoa huduma bora, salama na kwa wakati kwa wakazi wote wa Pangani na maeneo jirani.
Amefafanua kuwa ujio wa madaktari hao ni sehemu ya jitihada za kupunguza changamoto ya upatikanaji wa huduma za kibingwa katika ngazi ya wilaya, pamoja na kusogeza huduma hizo karibu zaidi na wananchi.
Timu hiyo inajumuisha madaktari bingwa wa fani mbalimbali, zikiwemo magonjwa ya wanawake na uzazi, mifupa, upasuaji, mfumo wa mkojo, magonjwa ya moyo, watoto, pamoja na magonjwa ya ndani.
Huduma hizo zinatarajiwa kutolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Pangani, ambapo wananchi wamehimizwa kujitokeza kwa wingi ili kufaidika na fursa hiyo muhimu.