TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA HUDUMA ZA UPANDIKIZAJI VIUNGO, BMH NI CHACHU YA HATUA HIZO

Published: May 08, 2026
TANZANIA YAPIGA HATUA KUBWA HUDUMA ZA UPANDIKIZAJI VIUNGO, BMH NI CHACHU YA HATUA HIZO cover image

Jeremia Mwakyoma & Jeremia Mbwambo
Picha na Gladys Lukindo
DODOMA - MEI 6, 2026

Nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi zilizopiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma za tiba za ubobezi zikiwemo za upandikizaji viungo katika mwili wa binadamu.



Haya yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe wakati akifungua mkutano wa kwanza wa kimataifa wa huduma za upandikizaji viungo hapa nchini ulioandaliwa na Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM); Mkutano ulioziletaΒ  Taasisi mbalimbali za Afya, Wanataaluma na Wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania.



" Sasahivi tunatoa huduma za upandikizaji uloto kwa watu wenye saratani na magonjwa mengine ya damu, upandikizaji wa figo na sasa tunaelekea katika upandikizaji wa Inni na Moyo; kwasasa tuna watu zaidi ya 147 waliopandikizwa Figo hapahapa ndani ya nchi huku BMH ikiwa na mchango mkubwa katika hatua hiyo" alisisitiza Dkt. Magembe.



Dkt. Magembe aliongeza kuwa, huduma za upandikizaji viungo zina gharama kubwa ndio maana serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuja na mpango wa Bima ya Afya kwa wote na hivyo akatoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanajiunga na Bima ili hata wale wananchi wasio na uwezo wanufaike na huduma za Afya.



Naye Mkurugenzi Mtendaji wa BMH,Profesa Abel Makubi ameishkuru serikali kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa,huku akimshkuru Mganga mkuu wa serikali kutokana na kuibyesha ushirikiano wake katika.suala zima linalohusu sekta ya afya.



Profesa Makubi pia aliwashkuru wataalam wa sekta ya afya zaidi ya 150 kutoka mataifa mbalimbali waliohufhuria mkutano huo,huku akisisitiza lengo ni kubadilishana uzoefu katika masuala mazima ya matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi.



Alisema hospitali ya Benjamini Mkapa kwa kushirikiana na wadau wengine imeandaa mkutano huo ikiwa na makusudi ya kueleza mwelekeo wao kwenye suala zima la upandikizaji viungo.



Akiwakilisha Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Prof. Razack Lokina amesema kuwa UDOM itaendelea kutoa mchango wake wa kuandaa na kuzalisha wataalamu mabingwa katika maeneo ya huduma za upandikizaji Figo na Uloto; itaendelea kufanya tafiti katika kuboresha huduma za upandikizaji viungo.Β