TANZANIA YAPOKEA RASMI MRADI WA KIKANDA WA UPANDIKIZAJI ULOTO NA SAYANSI YA DAMU KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA.

Published: Sep 15, 2025
TANZANIA YAPOKEA RASMI MRADI WA KIKANDA WA UPANDIKIZAJI ULOTO NA SAYANSI YA DAMU KATIKA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA. cover image

Na Jeremia Mwakyoma
DODOMA - SEPTEMBA 4, 2025

Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango ameshuhudia Serikali ya Tanzania kupitia Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ikipokea kuwa mwenyeji wa ujenzi wa kituo cha Umahiri cha upandikizaji uloto na sayansi ya magonjwa ya damu cha Afrika mashariki kitakacho kuwa chini ya BMH.


Akiwa katika ziara ya kikazi ya siku moja hapo BMH ambapo alishuhudia makabidhiano hayo, Makamu wa Rais amesema ni matarajio ya Serikali kuwa kituo hiki pamoja na kuimarisha huduma za upandikizaji uloto kwa watoto wenye ugonjwa wa selimundu lakini kitasaidia kuongeza uzalishaji wa wataalamu katika nyanja hiyo kupitia mafunzo na utafiti utakaofanyika.

Nae Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Denis Londo amesema kuwa kuanzishwa kwa kituo hicho ni heshima kubwa kwa nchi yetu na BMH yenyewe kwani kitasaidia kutoa na kubadilishana uzoefu katika nchi hizi za ukanda wa Afrika Mashariki.

Kwa upande wake mwakilishi wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt. Erick Zeimana ameelezea kuwa kuidhinishwa kwa waraka wa kuanzishwa kwa Kituo hiki cha Umahiri cha Kanda ya Afrika Mashariki na Baraza la Mawaziri wa Kisekta linalohusika na Afya mnamo tarehe 9 Mei 2025 ni hatua muhimu sana ya mafanikio katika Sekta ya Afya kwa ukanda wa Afrika Mashariki.

Ameongeza kuwa suala hili linatoa ushahidi wa dhamira ya dhati kutoka kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusukuma mbele ajenda ya huduma za afya katika ukanda wa Afrika Mashariki.

"Mpango wa vipaumbele vya uwekezaji katika Sekta ya afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2018 hadi 2028 unahamasisha kuanzishwa kwa Vituo vya Umahiri vya Kanda, na kwa hakika huu ni utaratibu wa kuboresha upatikanaji wa elimu ya juu ya afya na huduma za kibingwa, hii inaonesha azma yetu ya pamoja kama Afrika Mashariki ya kushirikiana, kusaidiana na kujenga mustakabali bora wa kiafya kwa wananchi wote wa Afrika Mashariki" alimalizia Dkt. Erick Zeimana.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi ameishukuru Wizara ya Afya, Wizara ya Fedha na Wizara ya Afrika Mashariki kwa uratibu wao uliowezesha Jumuiya ya Afrika Mashariki kuipatia Tanzania uenyeji wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Damu cha Afrika Mashariki kitakachojengwa hapo BMH.

"Kituo hiki kitasaidia kuleta mapinduzi ya matibabu ya ugonjwa wa sikoseli kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati" aliongeza Prof. Makubi

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya BMH Prof. Edward Hosea alimalizia kwa kuiomba Serikali isaidie upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha kimkakati cha Umahiri cha upandikizaji uloto na sayansi ya magonjwa ya Damu.