HAYATI RAIS BENJAMIN MKAPA ALIACHA ALAMA KATIKA HUDUMA ZA MATIBABU YA FIGO
Ziara ya Mama Anna Mkapa BMH
Na Jeremiah Mwakyoma , 10/02/2026, Dodoma.
Katika kuelekea hitimisho la Maadhimisho ya miaka 10 ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ifikapo 08 Mei 2026,Β Mheshimiwa Mama Anna Mkapa ametembelea Hospitali hiyo na kujionea mabadiliko makubwa katika huduma za kibingwa bobezi hasa Upandikizaji viungo.
Katika taarifa yake , Mama Anna Mkapa ameeleza jinsi ambavyo aliambatana na Hayati Benjamin Mkapa , Rais wa awamu ya tatu huko Japan na kuweza kuongea na marafiki ikiwemo Shirika la binafsi la TOKUSHUKAI, ambalo ndilo liliwezesha kuanzishwa kwa huduma za usafishaji figo (Dialysis) katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) na baadae BMH na sasa kufika hatua ya Upandikizaji Figo .
"Wakati Hayati Rais Mkapa anakwenda Japan na mimi nilikuwepo, leo ninafuraha kusikia hatua kubwa zilizopigwa kufikia hatua ya kupandikiza figo" alisisitiza Mheshimiwa Mama Anna Mkapa naΒ kupongeza juhudi za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mheshimwa Rais, Dr Samia Suluhi Hassan ambaye amewezesha huduma hizo kupanuka na kuwawezesha Wananchi Wengi kupata huduma.
Akimkaribisha Mama Anna Mkapa, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof Abel Makubi ameshukuru sana mchango wa Hayati Benjamin William Mkapa na kufafanua kuwaΒ maono yake yameacha alama kubwa katika huduma za matibabu ya Figo hapa nchini ambapo kwa sasa chini ya Mhe Dr Samia Suluh Hassan mpango unakamilishwa ili kujenga kituo cha Kikanda cha umahiri cha matibabu na mafunzo ya huduma za Upandikizaji Figo .
"Mpaka sasa Wananchi 54 wameshapandikizwa Figo na kati ya hao, asilimia 97% wanaendelea vizuri" aliongezea Prof. Makubi.
Mheshimiwa Mama Anna Mkapa ameahidi kuendelea kuunga mkono maboresho ya huduma hizo za Figo kupitia marafiki zake.
Β