WAZIRI WA KILIMO NA USALAMA WA CHAKULA WA JAMHURI YA SUDAN KUSINI MHE. CLEMENT JUMA MBUGONIWIA (MB) ARIDHISHWA NA UBORA WA HUDUMA BMH
Na Jeremia Mwakyoma, Jeremiah Mbwambo
PICHA: GLADYS LUKINDO - DODOMA JULAI 6, 2026
Waziri huyo wa Kilimo na Usalama wa Chakula wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Clement Mbugoniwia ambaye yupo hapa nchini kwa mwaliko wa Wizara ya Kilimo, baada ya kutembelea Maonesho ya Kitaifa na Kimataifa ya Kilimo alipata fursa ya kutembelea Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ambapo alipongeza Serikali ya Tanzania kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu, vifaa tiba, Wataalamu na kuridhishwa na ubora wa huduma za kibobezi zinazotolewa hapo BMH.
"Tunayo fursa ya mashirikiano kati ya nchi zetu za Tanzania na Jamhuri ya Sudan Kusini katika sekta ya Afya na Tiba Utalii, nitafikisha ujumbe kwa Serikali ya Sudan Kusini kupitia kwa Waziri wa Afya wa Sudan Kusini, nina uhakika viongozi wa Wizara ya Afya watapata nafasi ya kutembelea BMH, kujionea huduma zilizopo na hatimae kuanzisha mashirikiano katika sekta ya Afya" alisisitiza Waziri Mbugoniwia.
Aliongeza kuwa lengo la Serikali ya Sudan Kusini katika Afya linafanana na serikali ya Tanzani la kuwahudumia wananchi wake kuhakikisha wanapata huduma bora za Afya.
"Nchini kwetu Sudan Kusini tumekuwa tukitumia fedha nyingi kupeleka wananchi wetu nchi za Asia na maeneo mengine ya mbali Duniani kutafuta huduma za Kibobezi za Afya, lakini wenzetu Tanzania wana hospitali kubwa kama BMH, yenye miundombinu ya kisasa, vifaa tiba, Wataalamu wa kutosha na huduma bora za kibobezi hatuna haja sana ya kupeleka wananchi wetu Asia badala yake tunaweza kuwaleta hapa BMH" alibainisha Waziri Mbugoniwia.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa BMH Prof. Abel Makubi amesema kuwa BMH iko tayari kuanza kushirikiana na nchi ya Sudan Kusini kupitia Wizara ya Afya na anawakaribisha Sudan Kusini kuja kuona utoaji huduma, kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuona maeneo ya ushirikiano ikiwemo huduma za Tiba Utalii.
"Tukishirikiana na Chuo Kikuu cha Dodoma tunawakaribisha Wataalamu wa Afya kutoka Sudan Kusini kuja BMH kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo , mafunzo ya Ubingwa wa Juu katika taaluma za Afya kwa kuzingatia BMH ni Hospitali kubwa iliyojikita katika utoaji huduma za Afya, mafunzo na Tafiti" alisisitiza Prof. Makubi.
Prof. Makubi alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali kwa uwekezaji hospitalini hapo na kufanikiwa kuanzisha huduma 20 za ubingwa na 17 za kibobezi ambazo karibu asilimia 70 ya huduma hizo zikiwa zimeanzishwa wakati wa uongozi wa awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan.