SERIKALI YA MKOA WA SINGIDA KUWEKA PROGRAMU YA KUWAITA MADAKTARI BINGWA WABOBEZI WA BMH KUTOA MATIBABU KWENYE WILAYA ZA MKOA WA SINGIDA
Na Jeremia Mwakyoma
SINGIDA - FEB 27, 2026
Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Halima Dendego amesema kuwa Mkoa wa Singida utaweka programu ya kuwaita Madaktari Bingwa Wabobezi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) kwenda Mkoani Singida kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida kutoa Matibabu kwenye Wilaya za Mkoa huo.
"Kambi hizo za uchunguzi na matibabu zitatumika pia kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya kwenye Hospitali za Wilaya na Mkoa wetu wa Singida" alisisitiza Mhe. Dendego.
Mhe. Dendego alibainisha hayo wakati wa kikao kifupi cha kuwashukuru na kuwaaga timu ya Madaktari Bingwa Bobezi wa BMH walioweka kambi ya uchunguzi na matibabu wilayani Iramba kwa muda wa wiki moja kuanzia Feb 23 hadi 27, 2026.
Katika Kambi hiyo, BMH ilipeleka Wilayani Iramba madaktari Bingwa Wabobezi wa upasuaji, mfumo wa Mkojo, magonjwa ya moyo kwa watoto, magonjwa ya moyo kwa watu wazima, Upasuaji Mifupa na ajali, magonjwa ya akina mama na uzazi, masikio, pua na koo na magonjwa ya ndani.