MTINDO WA MAISHA USIOFAA HUCHANGIA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZWA

Published: May 14, 2026
MTINDO WA MAISHA USIOFAA HUCHANGIA MAGONJWA YASIYO AMBUKIZWA cover image

Na Jeremia Mwakyoma I Picha na Jeremia Mbwambo

MEI 13, 2026

 

Mtindo wa maisha usiofaa huchangia kwa kiasi kikubwa kusababisha kuongezeka kwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza (NCDs). Hayo yameelezwa na Mfiziotherapia wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) Bi. Magreth Raphael wakati wa kikao cha elimu ya masuala ya Afya akiangazia mfumo wa maisha unavyoweza kuchangia magonjwa yasiyo ya kuambukiza na namna gani Hospitali zinavyoweza kusaidia kutoka kuwa eneo la matibabu kufikia ustawi kamili wa Afya kimwili, kiakili na kijamii.

 

"Mfumo wa maisha usiofaa kwa kiasi kikubwa unasababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza ambayo yanachangia idadi kubwa ya vifo duniani, karibu asilimia 78 ya vifo vinasababishwa na magonjwa yasiyo ya kuambukiza" alisisitiza Bi. Magreth Raphael.

 

Alifafanua kuwa uamuzi wa kubadilisha tabia na mtindo usiofaa wa maisha ni uamuzi wenye gharama nafuu na hauna athari zaidi ya manufaa na hospitali zinaweza kubadilika kutoka kutoa huduma za kutibu maradhi (curative services) kwenda katika huduma za kukinga maradhi (preventive services)

 

Bi Magreth amesema kuwa jamii ifanye mabadiliko ya mtindo wa maisha ikiwa ni kuhakikisha mtu unakula mlo bora, unafanya mazoezi ya mwili angalau kwa nusu saa kwa siku, kuondoa msongo wa mawazo, kulala vizuri na kupata usingizi mzuri kati ya masaa 7 hadi 9 kila siku, kuacha matumizi ya pombe, sigara (tumbaku), dawa za kulevya na kuwa na mahusiano chanya kwenye jamii (positive social support.

 

Nae mtaalamu wa Tiba Lishe wa BMH Bw. Perfect Kikiwa amefafanua kuwa ulaji wa vyakula vyenye Karoli nyingi, Mafuta mengi, Sukari na Chumvi nyingi (Junk Food), vyakula vya kusindikwa na matumizi ya pombe kupitiliza ambayo hupelekea uzito kupitiliza na hatari ya magonjwa ya Kisukari, Shinikizo la Juu la damu, Saratani, magonjwa ya moyo, figo na inni.

 

Kikiwa amesisitiza matumizi ya mboga za majani na matunda na vyakula vya asili ambavyo havijasindikwa.