Mwanzo / Huduma Zetu / MKE WA RAIS WA ZANZIBAR MAMA MARIAM MWINYI ATEMBELEA BANDA LA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KWENYE MAONESHO YA WIKI YA AFYA ZANZIBAR, AIPA KONGOLE BMH KWA PROGRAMU ZA HUDUMA MKOBA NA TIBA UTALII.

MKE WA RAIS WA ZANZIBAR MAMA MARIAM MWINYI ATEMBELEA BANDA LA HOSPITALI YA BENJAMIN MKAPA KWENYE MAONESHO YA WIKI YA AFYA ZANZIBAR, AIPA KONGOLE BMH KWA PROGRAMU ZA HUDUMA MKOBA NA TIBA UTALII.

Published on May 12, 2025

Article cover image

Na Jeremia Mwakyoma
UNGUJA – MEI 8, 2025

Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi leo ametembelea banda la Maonesho la Hospitali ya Benjamin Mkapa kwenye Maonesho ya Wiki ya Afya  Zanzibar (Zanzibar Afya Week; Conference, Expo and Awards) yanayoendelea kufanyika katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo Unguja.

Wakati wa Ziara yake hiyo Mama Mariam Mwinyi ambaye pia ni Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation ametoa pongezi zake kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa hatua kubwa ilizozipiga katika utoaji wa Huduma za Ubingwa na Ubingwa wa Juu za Afya hapa nchini ambazo zinasaidia kupunguza Idadi ya Wananchi wanaokwenda nje ya nchi kutafuta huduma za aina hiyo, Aidha ameipongeza BMH kwa kuendesha Programu za Kambi za Matibabu na Tiba Utalii.

Hongereni kwa kuweza kushiriki katika maonesho haya ya Zanzibar Afya Week na pia hongereni Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuendelea kuboresha huduma zenu za Afya kwa matibabu hayo ya Ubingwa na Ubingwa wa Juu hapa nchini na kuzitangaza huduma hizo na kuzifikisha kwa Wananchi kupitia Huduma Mkoba na Tiba Utalii” alipongeza Mama Mariam Mwinyi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Mfumo wa Mkojo na Uzazi kwa Wanaume Said Mawji amemfahamisha Mama Mariam Mwinyi kuwa ili kupeleka huduma za BMH karibu zaidi na Wananchi, BMH huwa inaandaa kambi maalumu za matibabu kwenye maeneo ya Wananchi kwenye Mikoa mbalimbali (huduma Mkoba - Outreach Programs)  na mwitikio wa wananchi huwa ni mkubwa.

“Tayari tumeshafanya huduma mkoba (Kambi za uchunguzi na matibabu) 72 kwenye mikoa ya Dodoma, Tanga, Katavi, Manyara, Iringa, Njombe, Tabora na Zanzibar tumeshafika pia; na katika Kambi hizo tumefanikiwa kuwahudumia zaidi ya Wananchi 18,500” alifafanua Dkt. Mawji.

Dkt. Mawji alimalizia maelezo yake kwa kumjulisha Mama Mariam Mwinyi kuwa, kupitia Huduma za Afya za Ubingwa na Ubingwa wa Juu, BMH imekuwa ikitekeleza Programu ya Tiba Utalii kwa Wagonjwa kutoka nje ya Nchi ikijumuisha Mataifa kama Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia, Burundi, Comoro, Uturuki, Marekani, Uholanzi, Austria na baadhi ya Nchi za Mashariki ya Kati (Kuwait).