Magonjwa ya Kuambukiza
Published on July 08, 2025

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) inatoa huduma maalum za kinga, uchunguzi, matibabu na usimamizi wa magonjwa ya kuambukiza. Ikiwa na timu yenye ujuzi ya madaktari bingwa wa magonjwa ya kuambukiza, wanasayansi wa maabara, na watumishi wa kusaidia, BMH inatoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wa kulazwa kwa kutumia mbinu shirikishi na inayomlenga mgonjwa.
Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza hushirikiana kwa karibu na idara nyingine kama vile Tiba ya Ndani, Watoto, Famasia, Huduma za Maabara, na Afya ya Umma ili kuhakikisha huduma kwa wakati na yenye ufanisi. Huduma zinazotolewa ni pamoja na ushauri wa kitabibu, vipimo vya maabara, tiba ya viuavijasumu, usimamizi wa maambukizi nyemelezi, ufuatiliaji wa waliokutana na mgonjwa, kinga na udhibiti wa maambukizi (IPC), na elimu ya afya.
Makundi Makuu ya Magonjwa ya Kuambukiza Yanayotibiwa BMH
VVU/UKIMWI
BMH inatoa huduma kamili za VVU kupitia Kliniki ya Huduma na Matibabu (CTC), ikijumuisha tiba ya kufubaza virusi (ART), ufuatiliaji wa mzigo wa virusi, ushauri wa ufuasi wa tiba, na usimamizi wa matatizo yanayohusiana na VVU.
Kifua Kikuu (TB)
Uchunguzi na matibabu ya kifua kikuu kinachokubali dawa na kisichokubali dawa hupatikana, ikiwa ni pamoja na vipimo vya GeneXpert na tiba ya uangalizi wa moja kwa moja (DOT). BMH pia hushirikiana na programu za kitaifa za kifua kikuu kwa ufuatiliaji wa waliokutana na wagonjwa na kuwasaidia wagonjwa.
Hepatitis B na C
Hospitali hutoa huduma za uchunguzi, chanjo, na tiba ya dawa za kupunguza virusi kwa hepatitis B na C, pamoja na ufuatiliaji wa ini kwa ukawaida.
Malaria
Kwa kutumia vipimo vya haraka (RDTs) na hadubini, BMH hutambua na kutibu malaria kwa ufanisi, kwa kufuata miongozo ya kitaifa ya matibabu.
Magonjwa Yanayoibuka na Yanarudi Tena
BMH imejiandaa kushughulikia milipuko ya magonjwa kama vile UVIKO-19, kipindupindu, na dengue. Hospitali ina maeneo ya kutenga wagonjwa na timu za dharura kwa ajili ya kudhibiti na kutibu kwa ufanisi.
Maambukizi Yanayopatikana Hospitalini (HAIs)
Timu ya Kinga na Udhibiti wa Maambukizi husimamia kuzuia, kugundua, na kukabiliana na maambukizi yanayotokea ndani ya mazingira ya hospitali, ili kuhakikisha usalama wa wagonjwa na wafanyakazi.
Mipango ya Baadaye
BMH inalenga kupanua huduma zake za magonjwa ya kuambukiza kupitia:
-
Kuanzisha Kituo Mahiri cha Magonjwa ya Kuambukiza.
-
Kuimarisha ufuatiliaji wa magonjwa na maandalizi ya kukabiliana na milipuko.
-
Kuletea hospitali majukwaa ya kisasa ya uchunguzi yakiwemo ya uchunguzi wa kinasaba (molecular diagnostics).
-
Kuongeza mafunzo na tafiti kuhusu magonjwa ya kuambukiza kwa kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa.
-
Kuongeza chanjo na programu za utoaji elimu kwa jamii.
Hitimisho
Hospitali ya Benjamin Mkapa inaendelea kuwa sehemu muhimu ya mapambano dhidi ya magonjwa ya kuambukiza nchini Tanzania. Kupitia miundombinu ya kisasa, wafanyakazi wenye ujuzi, na dhamira ya kutoa huduma bora, BMH inasalia kuwa hospitali ya rufaa inayotegemewa kwa usimamizi wa magonjwa ya kuambukiza. Kwa mipango ya kupanua huduma na uwezo wake, hospitali iko katika nafasi nzuri kukabiliana na changamoto za sasa na zijazo za afya ya jamii.